Wednesday, May 2, 2012

NECTA yapunguza adhabu kwa waliofutiwa mitihani

Habari News Tanzania
 BARAZA la Mitihani la Tanzania (NECTA) limepunguza adhabu ya wanafunzi 3,303 waliofutiwa matokeo ya mitihani ya Kidato cha Nne na Maarifa kwa mwaka jana ya kutowaruhusu kufanya mtihani kwa miaka mitatu na kuwa mwaka mmoja.

Aidha, watahiniwa wote waliofanya udanganyifu na kufutiwa matokeo yao, wataruhusiwa kufanya mtihani wa Kidato cha Nne kama watahiniwa wa kujitegemea kuanzia mwaka ujao, 2013.

Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dk. Joyce Ndalichako aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuwa alisema uamuzi wa kupunguzwa kwa adhabu hiyo yamezingatia ubinadamu na uhusiano kwa wananchi baada ya walioathirika na adhabu hiyo kuomba msamaha.

Kuhusu chanzo cha udanganyifu, Dk. Ndalichako alisema matokeo ya awali ya uchunguzi yanaeleza kuteuliwa kwa wasimamizi wasiokuwa na sifa zinazotakiwa kama vile uzoefu kazini au kutokuwa na mafunzo ya ualimu.

Alisema pia wasimamizi wengine walipangiwa kusimamia mtihani katika shule wanazofundisha huku baadhi yao wakipewa taarifa za kusimamia vituo miezi miwili kabla ya kufanyika mitihani kinyume cha utaratibu.

Alitaja sababu nyingine ya udanganyifu ilikuwa baadhi ya wakuu wa shule kuingia katika vyumba vya mitihani kinyume cha taratibu za usimamizi huku baadhi yao wakishiriki katika kufanya maswali ya mitihani, jambo lililotoa mwanya kuyajua maswali na hatimaye kuingiza majibu ndani ya vyumba vya mitihani.

No comments: